Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Idara ya Uhusiano wa Umma ya Hizbullah imekanusha madai yaliyotolewa na mmoja wa viongozi wa kisiasa kuhusu eti Hizbullah imechukua misimamo inayokwenda kinyume na misingi yake ya kudumu na mitazamo yake iliyo wazi. Aidha, imesisitiza kuwa misimamo ya Hizbullah katika mafaili yote ni ya pamoja, yenye umoja na isiyobadilika.
Katika taarifa iliyotolewa Ijumaa tarehe 26 Tir (July 17 2026), Idara ya Uhusiano wa Umma ya Hizbullah ilisema: "Katika siku za hivi karibuni, baadhi ya vyombo vya habari vimechapisha mfululizo wa habari kuhusu misimamo inayodaiwa kuchukuliwa na baadhi ya viongozi wa Hizbullah katika kikao chao na Rais wa nchi; misimamo ambayo inadaiwa kwenda kinyume na misingi ya kudumu pamoja na mitazamo iliyo wazi na iliyotangazwa rasmi na Hizbullah. Jana pia, mmoja wa viongozi wa kisiasa, wakati wa kipindi cha mahojiano katika moja ya vituo vya televisheni vya Lebanon, alirudia madai hayo."
Taarifa hiyo iliongeza: "Idara ya Uhusiano wa Umma ya Hizbullah inasisitiza kuwa; madai yote yaliyotolewa kuhusu suala hili ni ya uongo mtupu na hayana msingi wowote, iwe kwa ujumla wake au kwa maelezo yake. Vilevile, tunasisitiza kuwa misimamo ya Hizbullah, iwe ile inayotangazwa hadharani au ile inayojadiliwa katika vikao vya ndani, ni ya pamoja na thabiti katika masuala yote."
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa; hali hiyo inahusu pia msimamo wa Hizbullah kuhusu kuiunga mkono Ghaza, ambao ni msimamo wa kimsingi, wa kidini, wa kimaadili na wa kibinadamu, na ambao Hizbullah inajivunia kuushikilia. Kadhalika, inahusu msimamo wake wa kukataa kabisa kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na adui Israel.
Maoni yako